Mark 11

Yesu Aingia Yerusalemu Kwa Shangwe

(Mathayo 21:1-11; Luka 19:28-40; Yohana 12:12-19)

1 aWalipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage na Bethania katika Mlima wa Mizeituni. Yesu akawatuma wawili wa wanafunzi wake, 2 bakawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu. Na hapo mtakapoingia kijijini, mtamkuta mwana-punda amefungwa hapo, ambaye hajapandwa na mtu bado. Mfungueni, mkamlete hapa. 3 cKama mtu yeyote akiwauliza, ‘Mbona mnamfungua?’ Mwambieni, ‘Bwana anamhitaji, na atamrudisha hapa baada ya muda mfupi.’ ”

4 dWakaenda, wakamkuta mwana-punda amefungwa kando ya barabara, karibu na mlango wa nyumba. 5Walipokuwa wanamfungua, watu waliokuwa wamesimama karibu wakawauliza, “Mna maana gani mnapomfungua huyo mwana-punda?” 6Wakawajibu kama vile Yesu alivyokuwa amewaagiza, nao wale watu wakawaruhusu. 7Kisha wakamleta huyo mwana-punda kwa Yesu na kutandika mavazi yao juu yake, naye akampanda. 8 eWatu wengi wakatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakatandaza matawi waliyokuwa wamekata mashambani. 9 fKisha wale waliokuwa wametangulia mbele na wale waliokuwa wakifuata nyuma wakapaza sauti, wakisema,

“Hosana!”
Kiebrania kusema Okoa, basi likawa neno la shangwe.


“Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!”

10 h“Umebarikiwa Ufalme unaokuja wa baba yetu Daudi!”

“Hosana kwake yeye aliye juu!”
11 iYesu akaingia Yerusalemu na kwenda Hekaluni. Akaangalia kila kitu kilichokuwamo, lakini kwa kuwa ilishakuwa jioni, akaenda zake Bethania pamoja na wale kumi na wawili.

Yesu Alaani Mtini Usiozaa

(Mathayo 21:18-19)

12 jKesho yake walipokuwa wakitoka Bethania, Yesu alikuwa na njaa. 13Akauona mtini kwa mbali, naye akaenda ili aone kama ulikuwa na matunda. Alipoufikia, akakuta una majani tu, kwa kuwa hayakuwa majira ya tini. 14 kAkauambia ule mti, “Tangu leo mtu yeyote asile kamwe matunda kutoka kwako.” Wanafunzi wake walimsikia akisema hayo.

Yesu Atakasa Hekalu

(Mathayo 21:12-17; Luka 19:45-48; Yohana 2:13-22)

15 lWalipofika Yerusalemu, Yesu akaingia katika eneo la Hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakinunua na kuuza humo ndani. Akazipindua meza za wale waliokuwa wakibadilisha fedha, na pia viti vya wale waliokuwa wakiuza njiwa, 16wala hakumruhusu mtu yeyote kuchukua bidhaa kupitia ukumbi wa Hekalu. 17 mNaye alipokuwa akiwafundisha, akasema, “Je, haikuandikwa kuwa:

“ ‘Nyumba yangu itaitwa
nyumba ya sala kwa mataifa yote’?
Lakini ninyi mmeifanya kuwa ‘pango la wanyangʼanyi.’ ”

18 nViongozi wa makuhani na walimu wa sheria wakapata habari hizi, nao wakaanza kutafuta njia ya kumuua, kwa kuwa walikuwa wakimwogopa, kwa sababu umati wote ulikuwa unashangazwa na mafundisho yake.

19 oIlipofika jioni, Yesu na wanafunzi wake wakatoka nje ya mji.

Mtini Ulionyauka

(Mathayo 21:20-22)

20 pAsubuhi yake walipokuwa wakipita, wakauona ule mtini umenyauka kutoka juu hadi kwenye mizizi yake. 21 qPetro akakumbuka na kumwambia Yesu, “Rabi, tazama! Ule mtini ulioulaani umenyauka!”

22 rYesu akawajibu, “Mwaminini Mungu. 23 sAmin, nawaambia, mtu yeyote atakayeuambia mlima huu, ‘Ngʼoka ukatupwe baharini,’ wala asione shaka moyoni mwake, bali aamini kwamba hayo asemayo yametukia, atatimiziwa. 24 tKwa sababu hiyo nawaambia, yoyote mtakayoyaomba mkisali, aminini ya kwamba mmeyapokea, nayo yatakuwa yenu. 25 uNanyi kila msimamapo kusali, sameheni mkiwa na neno na mtu, ili naye Baba yenu aliye mbinguni awasamehe ninyi makosa yenu. [ 26 vLakini kama ninyi msiposamehe, wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu.]”

Swali Kuhusu Mamlaka Ya Yesu

(Mathayo 21:23-27; Luka 20:1-8)

27 wWakafika tena Yerusalemu, na Yesu alipokuwa akitembea Hekaluni, viongozi wa makuhani, walimu wa sheria pamoja na wazee wa watu wakamjia. 28Wakamuuliza, “Unafanya mambo haya kwa mamlaka gani? Na ni nani aliyekupa mamlaka ya kufanya hayo?”

29Yesu akawajibu, “Nitawauliza swali moja. Nijibuni, nami nitawaambia ni kwa mamlaka gani ninafanya mambo haya. 30Niambieni, je, ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni au kwa wanadamu?”

31Wakahojiana wao kwa wao, wakisema, “Kama tukisema, ‘Ulitoka mbinguni,’ atatuuliza, ‘Mbona hamkumwamini?’ 32 xLakini tukisema, ‘Ulitoka kwa wanadamu,’…” (Waliwaogopa watu, kwa sababu kila mtu aliamini kwamba Yohana alikuwa nabii wa kweli.)

33Kwa hiyo wakamjibu Yesu, “Hatujui.”

Naye Yesu akawaambia, “Wala mimi sitawaambia ni kwa mamlaka gani ninatenda mambo haya.”

Copyright information for SwhNEN